Search This Blog

Friday, May 6, 2016

ALIYEPARAMIA UKUTA WA IKULU KENYA AKUTWA AMEKUFA BAADA YA KUACHIWA NA MAHAKAMA


MWANAMUME aliyekamatwa baada ya kuingia katika Ikulu ya rais jijini Nairobi bila idhini alizikwa Alhamisi nyumbani kwao katika kijiji cha Mutuini kilichoko Dagoreti Kaunti ya Kiambu.

William Ngene Njuguna aliyekuwa na umri wa miaka 28 alipatikana ameuwawa katika bustani ya Uhuru mjini Nairobi siku mbili baada ya kuachiliwa kutokana na kesi ya kuingia kwake ikuluni, lakini familia ya marehemu inatilia shaka chanzo cha kifo chake.
“Njuguna alipatikana akiwa na majeraha kichwani na jicho lake la kushoto haliko. Huenda ikawa alipigwa risasi kichwani,” alisema amu yake William Ngene.
Katika mazishi yake yaliyohudhuriwa na jamaa na marafiki pamoja na mwakilishi wa wadi wa eneo hilo, Bw Martin Karanja, marehemu alikumbukwa kuwa mtu aliyesema mengi na aliyewashangaza wengi kwa yale aliyoongea.

“Kila aliposimama kuzungumza, yaliyotoka kinywani mwake yalikuwa ya kushangaza. Alidai kuwa dreamer. Ni ndoto zake zilizompeleka kuingia ikuluni. Wengi hawakumtilia maanani,” alisema rafiki yake, Bw Peter Mbugua.

Kulingana na familia yake, Njuguna alikuwa amepanga kuingia katika ikulu ya rais kwa muda mrefu. Baada ya kufunga kwa maombi kwa siku 40, mpango wake ulipokamilika, aliiarifu familia yake na kuwaaga na kuelekea ikuluni alipokamatwa na maafisa wa GSU baada ya kuuruka ukuta.
Sikio la kufa...
“Tulijaribu kumkanya dhidi ya mpango wake wa kwenda ikuluni lakini alisisitiza kuwa ni jambo la pekee alilobakisha kufanya maishani mwake na lazima angeingia ikuluni ili aione kwa macho yake mwenyewe. Kile alichotaka sana ni kumsalimu rais Uhuru Kenyatta,” alisema Bw Mbugua.

Familia yake ilipata ripoti ya kifo chake kupitia maafisa wa uchunguzi bungeni. Aidha, ripoti za ukaguzi wa maiti uliofanywa zilidhihirisha kuwa Ngene aliuawa baada ya kupigwa kwa silaha butu kichwani. Hata hivyo, familia yake haikufurahishwa na jinsi ukaguzi wa mwili wake ulivyofanywa.
“Stakabadhi tulizopewa tusahihishe zilikutambua mwili wake katika chumba cha kuhifadhi maiti ya city ni tofauti na zile tulizopewa wakati wa ukaguzi wa mwili. Hatukushirikishwa wakati wa ukaguzi wa mwili wake,” alisema mjombake marehemu, Bw George Mwaura.

Kwa sasa familia hiyo inataka uchunguzi wa kina ufanywe ilikubaini chanzo cha kifo cha Njuguna. Njuguna ambaye alikuwa mtoto watatu katika familia yake hakuwa na mke wala mtoto. Amewaacha wazazi wake na ndugu zake watatu.

Share:

0 comments:

Post a Comment