Search This Blog

Tuesday, May 3, 2016

KAMATI YA KUICHUNGUZA LUGUMI HAIJAANZA KAZI, CHANGAMOTO ZATAJWA


Kamati ndogo ya wabunge tisa iliyoundwa kuchunguza sakata la kampuni ya Lugumi Enteprises Ltd na Jeshi la Polisi haijaanza kazi, huku ikitakiwa kutekeleza majukumu tofauti na hadidu za rejea, Mwananchi limeelezwa.
Lugumi imeingia kwenye mzozo baada ya kubainika kuwa ilifunga mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole kwenye vituo 14 tu, tofauti na mkataba ilioingia na Jeshi la Polisi mwaka 2011 unaotaka zifungwe kwenye vituo 108.
Licha ya kushindwa kufunga mashine hizo, kampuni hiyo ililipwa asilimia 99 ya fedha zote kwenye mradi huo uliogharimu Sh37 bilioni.
Habari kutoka ndani ya kamati hiyo iliyoundwa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), zinaeleza kuwa kuchelewa kuanza kazi ni mpango mahususi utakaotoa mwanya kwa Lugumi kufunga mashine hizo kwenye vituo vilivyosalia. Kamati hiyo ndogo imepewa jukumu la kuchunguza utekelezaji wa mkataba ambao Jeshi la Polisi iliingia na Lugumi na ilisema kuwa itakuwa ikifanya ziara vituoni kwa kushtukiza, ili kuondoa uwezekano wa kampuni hiyo kupata habari itakakotembelea na kupeleka mashine mapema.
“Unajua ni lazima kamati ipewe fedha pamoja na mahitaji mengine kwa ajili ya kuanza kazi. Mpaka sasa haijapewa chochote na Bunge ikiwa imepita wiki nzima, licha ya kuwa kamati imejipanga kwa kila kitu,” alisema mmoja wa wabunge aliyeongea na Mwananchi kwa sharti la jina lake kusitiriwa.
“Watu tunaofanya nao kazi wanatueleza kuwa kuna vifaa vinafungwa kwenye vituo vya polisi, ili kamati ndogo ikienda ikute tayari vipo na kukwamisha uchunguzi. Ila hata kama watavifunga haitasaidia maana havitaweza kufanya kazi kwa sababu havijaunganishwa na mkongo wa taifa.”
Hata hivyo, naibu katibu wa Bunge, John Joel alilieleza gazeti hili jana kuwa tatizo si fedha.
“Kamati hii itaanza uchunguzi wake mkoani Dodoma. Ikimaliza hapa ndiyo itaendelea maeneo mengine. Tatizo siyo pesa inahitaji kuwa na watalaamu wa kuweza kuzitambua mashine hizo,” alisema Joel.
Katika ufafanuzi wake Joel alisisitiza kuwa jukumu la kamati hiyo ni kutembelea maeneo zilikofungwa mashine hizo, ili kutambua kama kweli zipo ama hazipo.
Baadhi ya hadidu za rejea ambazo kamati hiyo yenye wajumbe tisa ilitakiwa kuangalia ni kupata ukweli kama Lugumi ililipa kodi katika fedha ilizolipwa kutokana na mkataba huo, kupitia mfumo mzima wa utoaji zabuni, kuangalia uwezekano wa kampuni kuwa na sifa za kupewa kazi hiyo, kuangalia thamani ya vifaa vilivyonunuliwa na kazi hiyo kutolewa bila kushindanisha zabuni na hivyo kuifanya ipange gharama za juu.
“Unajua jambo hili ni zito. Sisi tulipewa hadidu zetu, lakini kwa sasa kamati ndogo inatakiwa kupita maeneo mbalimbali kuhakiki mashine hizo tu,” alisema mmoja wa viongozi wa kamati hiyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
“Kamati ndogo itafuatilia suala hili kulingana na majukumu iliyojipangia na ambayo tayari imeanza kuyatekeleza. Ikimaliza kazi itakabidhi ripoti kwa Spika. Kama Spika ataamua kuileta bungeni sawa au akiamua kutoileta kama ile ya sukari ambayo hoja yake ilianzia kwa (mbunge wa Kibamba, John) Mnyika, yote yatakuwa sawa ila kamati itakuwa imetekeleza wajibu wetu.”
Kamati hiyo iliyoundwa Aprili 23, pia ilijigawanya kwenye kamati ndogo tatu zitakazotawanyika sehemu tofauti kufanya kazi hiyo.
Habari hizo zinabainisha kuwa kama mashine hizo zitafungwa vituoni, hilo halitasaidia kwa sababu kamati ndogo itahoji kitendo cha kuzinunua na kuzisambaza wakati ikijulikana wazi kuwa haziwezi kufanya kazi.
“Ni lazima tuhoji kwa sababu manunuzi yanapofanyika lazima utaratibu unakuwa umewekwa na kumbuka mashine hizi zilinunuliwa kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi, sasa iweje ziwekwe halafu hazifanyi kazi? Kumbuka takribani miaka mitatu iliyopita PAC iliwahi kuhoji suala hili na kutoa miezi sita, lakini hakuna majibu ya maana yaliyotolewa,” alisema mjumbe mwingine.
Zinaeleza kuwa kamati hiyo ndogo pia itachunguza baadhi ya mambo ambayo hayakutolewa ufafanuzi wa kina na Jeshi la Polisi lilipoitwa mbele ya PAC kujibu hoja mbalimbali zilizotakana na maelekezo ya utekelezaji wa mkataba huo zilizowasilishwa na polisi.
Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hillaly alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema kwa sasa hawezi kusema jambo lolote kwa kuwa shughuli zote zinafanywa na kamati ndogo.

SOURCE
Share:

0 comments:

Post a Comment