Search This Blog

Wednesday, April 27, 2016

CAG AANIKA MAJIPU YALIYOIVA

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema wakati umefika sasa wa kubadili mfumo kutoka ule wa kutegemea vyombo vya serikali kutumika kuchunguza namna mafisadi walivyopata mali zao ili sasa mafisadi wenyewe ndio wathibitishe vyanzo vya mali hizo.
Amesema wanaposhindwa moja kwa moja, itambulike kwamba si mali za halali. Aidha, amesema staili ya kuliongoza Taifa inayofanywa na Rais John Magufuli, itasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza dharau iliyoanza kufanywa na watendaji wa serikali na hasa wenye vyeo vya juu katika utekelezaji wa maagizo yanayotolewa na CAG.
Profesa Assad aliyasema hayo akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuwasilisha taarifa yake ya ukaguzi ya mwaka 2014/2015 kwa kipindi kinachoishia Juni, 2015 mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, Kuhusu mafisadi kuthibitisha namna walivyopata mali zao, Profesa Assad alisema huo ni utaratibu unaotumika katika baadhi ya mataifa makubwa ikiwemo Marekani ambapo si jukumu la serikali kutafuta ushahidi wa namna kiongozi wa umma alivyopata mali, bali jukumu hilo linaachwa kwa mhusika mwenyewe kuithibitishia serikali.
“Yaani pale inapoonekana kiongozi amekuwa na mali za ghafla ambazo hazitoi uhalisia wa upatikanaji wake, kazi ya serikali inakuwa ni kumwagiza mhusika mwenyewe kueleza mchanganuo wa vyanzo vyake vya mapato vilivyomwezesha kuwa na mali hiyo.
“Utaratibu huu unatumika sana Marekani na kwa kiwango kikubwa umesaidia kuwafanya viongozi wa umma kuhofia kuwa na mali ambazo watashindwa kuzielezea namna walivyozipata hatua ambayo inasaidia sana kujenga nidhamu ya kuheshimu fedha za umma,” alisema Profesa Assad.
Staili ya Magufuli yamkuna Akizungumzia staili ya uongozi ya Rais Magufuli, alisema sauti ya Rais Magufuli imeanza kubadili nidhamu serikalini. Kutokana na hilo, Mdhibiti na Mkaguzi huyo wa Hesabu za Serikali alisema hakuna haja ya kuendelea kuipa meno zaidi taasisi hiyo, akipinga pia pendekezo lililotolewa kwamba ofisi ya CAG ipewe meno ya kuwashitaki moja kwa moja mahakamani viongozi wanaobainika kufanya ubadhirifu baada ya ukaguzi.
“Mimi sidhani kama ni vema kwa CAG kuwa na nguvu ya kukagua na wakati huo huo kuwapeleka mahakamani wahusika wa ubadhirifu. Kilichokuwa kinahitajika kwa nchi hii ilikuwa ni kupata ‘tone’ (sauti) ya kiongozi wa juu ili watendaji serikalini na hasa wa ngazi ya juu kabisa washituke.
“Kwa namna yoyote ili viongozi wa juu wakinyooka, mfumo utakwenda hivyo hadi katika ngazi ya chini kabisa na kwa hatua hiyo nchi itaheshimu mamlaka mbalimbali za nchi, ikiwa ni pamoja na kuheshimu mapendekezo ya CAG. Sasa ni dhahiri nchi imepata kiongozi mwenye ‘tone’ ya kuiweka nchi sawa,” alisema bila kumtaja Rais Magufuli.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa akikemea waziwazi uzembe, ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma na amekuwa akichukua hatua za kuwawajibisha viongozi wanaokutwa na kasoro hizo kupitia msemo aliouasisi na kupata umaarufu mkubwa wa utumbuaji wa majipu.
Alisema kutokana na mabadiliko ya kasi ya nidhamu katika utumishi wa umma, kazi inayofanywa na CAG ya kukagua na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa na serikali kutokana na ukaguzi wake, itaanza kuheshimika hatua itakayosaidia kupunguza wizi na ubadhirifu katika mali za umma.
Wabunge kuzihukumu Uda, Dart.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema mapendekezo yatakayotolewa na Bunge baada ya kupitia na kujadili ripoti ya CAG kuhusu mauzo ya hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) na ununuzi batili wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), utatekelezwa mara moja.
CAG katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2014/2015, aliyoiwasilisha bungeni juzi, ameshauri Uda lirudishwe chini ya usimamizi wa serikali na pia hatua zichukuliwe dhidi ya iliyokuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Uda na Mwenyekiti wake, Idd Simba kutokana na kukiuka taratibu za uuzaji wa hisa za shirika hilo.

SIMBACHAWENE NAYE ANENA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene aliliambia gazeti hili jana mjini hapa kuwa baada ya mjadala wa Bunge kuhusu ripoti ya CAG, serikali itachukua hatua stahiki katika suala la UDA na DART mara moja.
Kabla ya mauzo hayo ambayo sasa yanadaiwa kuwa ni tata ya hisa kwa kampuni binafsi ya Simon Group inayomilikiwa na Robert Kisena, Uda ilikuwa inamilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Saalaam.
Mradi wa DART pia upo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Simbachawene alisema kutokana na matakwa ya kikatiba, mara baada ya CAG kukamilisha kazi yake, hukabidhi ripoti hiyo kwa Rais ambaye naye huiwasilisha bungeni, hatua ambayo baadaye huanzisha mjadala wa umma, kujadili yaliyobainika na mapendekezo ya CAG kupitia ukaguzi wake.
“Kama inavyofahamika tayari ripoti ya CAG imefika bungeni, kinachofuata sasa ni Bunge kujadili kulingana na mapendekezo ya CAG na baadaye kutushauri sisi kama serikali hatua stahili za kuchukua kwa masuala yote,” alisema Simbachawene.
Alisema ni nia ya serikali kuona kuwa masuala ya Uda na DART, yanapata ufumbuzi wa kudumu ili kulinda maslahi ya umma kwa vile mashirika hayo yalianzishwa kwa kutumia fedha za wananchi.
“Suala la Uda limechukua muda mrefu sana na kumekuwepo na mapendekezo mengi sana yaliyowahi kutolewa na Bunge kwa suala hili, tunadhani sasa wakati umefika wa kuhakikisha kuwa tunalimaliza kabisa kwa kuzingatia maoni na ushauri wa CAG na Bunge,” alieleza Simbachawene.
LAAC NAYO YATOA NENO
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (LAAC), Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota (CCM) akizungumzia mapendekezo hayo ya CAG jana, alisema Bunge litafanya kazi ya kupitia hoja za CAG kuhusu Uda na Dart kwa weledi mkubwa.
“Suala la Uda ni suala nyeti, kwa vile CAG amekabidhi taarifa yake kwa Bunge, sasa sisi kama Kamati tutapata wasaa mzuri wa kulipitia suala hilo na lile la DART ili kuweza kulishauri Bunge na Serikali hatua stahiki za kuchukuliwa. Lengo ni kuhakikisha maslahi ya umma yanazingatiwa,” alisema Chikota.
Alisema wakati wa vikao vya Kamati vilivyofanyika Dar es Salaam, suala la Uda liliahirishwa kujadiliwa ili kuwapa wajumbe muda na nafasi zaidi ya kupitia taarifa mbalimbali za uuzaji wa hisa za shirika hilo na kuongeza kuwa taarifa ya CAG itawajengea uwezo zaidi kulijadili kwa kina na kutoa mapendekezo yenye maslahi kwa umma.
PAC NAYO YAFUNGUKA
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly (CCM) alisema; “Kwa sasa nisiseme mambo mengi maana ripoti yenyewe ya CAG ndiyo imefika bungeni, nadhani baada ya kuichambua kwa masuala mbalimbali ikiwemo hayo ya Uda na Dart, sisi kama Bunge tutaishauri serikali hatua muafaka za kuchukua.”
CAG JUU YA UDA
Dart Akizungumzia Uda, CAG alisema Bodi ya Wakurugenzi ya Uda iliuza hisa za shirika bila kupata kibali cha serikali. Alisema hisa za Shirika la Uda zilithaminishwa kwa bei ya Sh 744.79 kwa kila hisa Oktoba, 2009 na Novemba, 2010 thamani ya kila hisa ikawa Sh 656.15.
Alisema hata hivyo katika uuzaji huo, Bodi ya Wakurugenzi ya Uda ilitoa punguzo la asilimia 60 kwa kila hisa kwa Simon Group bila kuwepo na sababu za kufanya hivyo na kwamba kwa mujibu wa Mlipaji Mkuu wa Serikali, Serikali haitambui uuzwaji wa hisa hizo.
CAG alisema kulingana na Mkataba wa kuwasilisha hisa wa Februari 11, 2011, mnunuzi (Simon Group) atalipa jumla jumla ya Sh bilioni 1.14 kama bei ya ununuzi wa hisa zote ambazo zilikuwa hazijagawiwa, ingawa mkataba haukuonesha akaunti ya benki ambayo malipo yangefanyika.
Taarifa hiyo ilisema Simon Group alilipa kiasi cha Sh milioni 285 pekee katika akaunti namba 0J1021393700 ya Benki ya CRDB, inayomilikiwa na Uda na hakukuwa na malipo mengine ya ziada yaliyofanywa na mwekezaji kuhusu ununuzi wa hisa za Uda.
Alisema Mwenyekiti wa Bodi (Idd Simba) alipokea kiasi cha Sh milioni 320 kupitia akaunti yake binafsi kutoka kwa mwekezaji ambayo kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo ilikuwa ni ada ya ushauri alioutoa kwa mwekezaji jambo ambalo lilizua mgongano wa kimaslahi.
Kuhusu Dart, CAG alisema ukaguzi unaonesha kuwa upungufu umeendelea kuwapo katika kuzingatia sheria na kanuni za ununuzi, hivyo kuwapo kwa usimamizi mbovu wa mikataba.
Alisema ukaguzi ulibaini kutofuatwa kwa taratibu za ununuzi kama vile mabadiliko ya mikataba kutoidhinishwa na Bodi za Zabuni, ununuzi wa mabasi ya mwendo kasi zaidi ya mahitaji na kuchelewa kuanza kwa huduma ya mabasi hayo, mabasi yaliyonunuliwa ambayo hayajapokelewa kwa muda mrefu, ununuzi uliofanyika nje ya wazabuni waliothibitishwa na kuingia mikataba isiyokuwa na kikomo cha muda wa uwekezaji.


NEWSSOURCE=http://www.habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/9111-cag-awabana-mafisadi
Share:

6 comments: