Search This Blog

Monday, April 25, 2016

JE UKIMYA WA UKAWA BUNGENI NI WA KULINDA MASLAHI?


UAMUZI wa Kambi ya Upinzani bungeni kuingia katika vikao vya Bunge na kugeuka bubu wakati wa mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, umechukuliwa kwa hadhari kuwa unaweza kusababisha kambi hiyo ionekane inalinda posho bungeni.
Hadhari hiyo imetolewa na wasomi na viongozi mbalimbali waliozungumza na gazeti hili jana, walipokuwa wakitoa maoni kuhusu uamuzi wa kambi hiyo kususa hotuba hiyo.
Dk Bana
Mhadhiri wa fani ya siasa na utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana, ndiye aliyesema kuwa kama uamuzi huo wa kuwa bubu bungeni hautabadilishwa, kambi hiyo itaonekana inalinda posho na kwamba haipo kwa ajili ya kutetea wananchi.
“Kazi yao ni kuwakilisha wananchi na makundi yote bungeni, sasa kitendo cha kuota ububu na kushindwa kueleza kero za wananchi, ni kutotendea haki wananchi maana ni vema wakae bungeni na kutoa hoja zao la sivyo, itafika wakati watatuomba radhi wananchi,” alisisitiza.
Akizungumzia hoja ya kwanza ya Mwenyekiti wa kambi hiyo, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), kulalamikia muundo wa Serikali kutowekwa gazetini, Dk Bana alihoji kama Mbowe hajui kuwa muundo wa Serikali hautolewi kwa kila mtu.
Kuhusu suala la fedha zilizokatwa katika Mfuko wa Bunge na kuelekezwa katika utengenezaji wa madawati, Dk Bana aliwashangaa wawakilishi hao wa wananchi wanaopingana na uamuzi wa kumuinua mwananchi wa kawaida.
Alisema wananchi wote walipendezwa na hatua hiyo ya Serikali ya kuchukua fedha zilizotoka bungeni baada ya kubana matumizi na kupeleka katika kununua madawati.
“Hatua hii ni kielelezo kuwa Bunge lilikuwa likipangiwa fedha nyingi kuliko matumizi yake hivyo kusababisha kuwepo matumizi ya hovyo, sasa viongozi wa Bunge kuliona hilo na kurejeshwa kwenye jamii ni jambo jema,” alisema.
Alionya kuwa mikakati ya kambi ya upinzani, ni kutetea wananchi lakini kwenye hilo wananchi wenyewe kila kona wanawashangaa kwani inaonesha kutetea maslahi ya wabunge.
Bashiru Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema wananchi wanaangalia vitendo vya wabunge wao ndani ya Bunge na watawahukumu kwani michango yao ndani ya Bunge ni muhimu na njia ya kutatua tatizo si kususa, bali kufuata taratibu za kisheria.
Alisema uamuzi wa kutozungumza, unaondoa maana ya vyama vya upinzani ndani ya Bunge kwa kuwa watashindwa kujadili masuala yenye manufaa ya wananchi, kwani mawazo ya kiongozi wa upinzani bungeni ni muhimu na yanawekwa kwenye kumbukumbu.
“Kuwekwa kwenye kumbukumbu mawazo hayo ni kwa ajili ya vizazi vijavyo, sasa kitendo cha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kutumia vibaya nafasi anayopewa, ni udhaifu wa kimkakati,” alisisitiza Bashiru.

Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema wanavyofanya wapinzani ni jambo lisilopendeza katika kuleta umoja wa kitaifa, kwani wao ni wawakilishi wa wananchi ndani ya Bunge na kususa siyo jambo la kiungwana
Share:

0 comments:

Post a Comment