Search This Blog

Friday, April 29, 2016

MAPATO YA MADINI YAONGEZEKA TZ, BIL 6 HUPOTEA KILA MWAKA


Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji wa Uwazi Katika Mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (Teiti), Jaji Mark Bomani amesema bado Serikali inapoteza Sh6 bilioni kila mwaka katika mapato ya madini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa ripoti ya tano na sita za Teiti, Jaji Bomani alisema kiasi hicho kimepungua kutoka Sh66 bilioni zilizokuwa zikipotea hadi kufikia mwaka 2009, ilipotolewa ripoti ya kwanza ya kamati hiyo.
“Kwanza nakshi kati ya malipo yaliyosemekana yamefanywa na kampuni na fedha zilizokuwa zimepokelewa na Serikali, imezidi kupungua. Ripoti ya kwanza ya mwaka 2009 ilionyesha nakshi ya Dola za Marekani 30 milioni (Sh66 bilioni). Hii ilitushtua sana,” alisema Jaji Bomani na kuongeza:
“Angalau ripoti ya mwaka 2014 nakshi imeshuka hadi kufikia Sh6 bilioni. Jumla ya mapato ya Serikali yamepanda kutoka Sh28 bilioni hadi Sh1.2 trilioni, yaani ongezeko la takribani mara 10.”
Hata hivyo alisema licha ya ongezeko hilo bado mapato yangeongezeka zaidi, kama hatua zingechukuliwa.
“Kwa mfano hadi mwaka 2012 mrabaha unaotolewa na kampuni za madini ya dhahabu ulikuwa asilimia tatu. Kamati yangu ilipendekeza…kwanza asilimia ya mrahaba iongezwe kutoka asilimia tatu hadi angalau asilimia tano. Pili, mrabaha usiwe faida zilizopata hizo kampuni, bali jumla ya mauzo. Tofauti yake ni kubwa mno,” alisema Jaji Bomani.
Aliongeza kuwa Serikali ilitekeleza ushauri huo na kupandisha mrabaha huo, kutoka asilimia tatu hadi nne.
Hata hivyo alisema pendekezo lao la kutaka asilimia 60 ya mauzo ya kampuni za madini yarejeshwe nchini, halikukubaliwa.
“Kampuni za madini ya dhahabu kwenye mikataba maalumu ziliruhusiwa kuwekeza nje mauzo yake yao yote, kinyume na utaratibu wa kampuni nyingine ambazo hutakiwa kurejesha nchini mauzo yao,” alisema.
Alisema kwa bahati mbaya zaidi ruhusa hiyo imerasimishwa katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
“Utaratibu huu umeinyima Tanzania fursa ya kuongeza fedha za kigeni (foreign reserves) jambo linalochangia kuimarisha thamani ya shilingi. Naishauri Serikali kulitafakari suala hili hasa kwa kujua kwamba ni asilimia 20 tu ya madini yaliyogunduliwa ndiyo inachimbwa hadi leo. Bado asilimia 80 hayajachimbwa.”
Jaji Bomani ambaye alitumia fursa hiyo kustaafu nafasi yake ya uenyekiti wa kamati hiyo, aliishauri pia Serikali kupanua wigo wa wachimba madini kama vile wachimbaji wa kati ambao pato lao linazidi Sh200 milioni.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu, Ludovick Utouh aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ripoti hizo, alisema Serikali ilifanya makosa kuzimilikisha kampuni za madini migodi moja kwa moja.
‘Tunaweza kupata mapato zaidi ya madini kama tutaangalia umiliki. Mimi kama Utouh nasema utaratibu tulioutumia haukuwa sahihi. Botswana kwa mfano, ile dhana ya kusema Serikali haifanyi biashara haipo. Inatakiwa ifanye biashara kwa niaba ya wananchi wake. Tunatakiwa kuwa na wawakilishi wetu kwenye kampuni hizo, hata kwenye bodi zao,” alisema Utouh.
Alisema kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda rasilimali za nchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano kifungu cha 27 kinasema, kila mtu ana wajibu wa kutunza rasilimali za nchi… haya yanayozungumzwa hapa ni ya kisheria,” alisema Utouh.

Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment