SERIKALI imesema ipo tayari kuwasilisha bungeni baadhi ya mikataba ambayo itaonekana ina ulazima wa kufika bungeni ili kujadiliwa na wabunge kwa niaba ya wananchi kabla ya kupitishwa.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Kunti Majala (Chadema) aliyetaka kufahamu ni kwa nini serikali inapitisha mikataba bila kuiwasilisha bungeni.
Katika swali lake, Majala alisema kinyume cha matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoagiza mikataba kufikishwa bungeni ili kujadiliwa, serikali imekuwa ikipitisha mikataba hiyo bila kufanya hivyo.
Alisema pamoja na madhara mbalimbali, yanayosababishwa na hatua hiyo, pia nchi imekuwa inapata hasara kubwa kutokana na baadhi ya watendaji kupitisha mikataba hiyo kwa kushawishika na rushwa, hatua aliyosema imechangia kushamiri kwa vitendo vya ufisadi nchini.
Waziri Mkuu akijibu swali hilo, alikiri kuwa ni kweli Bunge lina wajibu wa kuisimamia serikali lakini yapo maeneo ambayo limetoa mamlaka ya kisheria kwa serikali kutekeleza majukumu mbalimbali ili kuharakisha maendeleo.
Alisema moja ya eneo ambalo wabunge kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametoa mamlaka kwa serikali kutekeleza majukumu yake ni katika eneo la mikataba, kwa Katiba kutoa nguvu ya kisheria kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia na kupitisha mikataba hiyo.
“Mwanasheria Mkuu anafanya kazi hii ya kupitia mikataba kwa niaba ya serikali na Bunge, kama mikataba yote ingekuwa inakuja hapa bungeni ili kujadiliwa na wabunge basi Bunge lisingekuwa na kazi nyingine zaidi ya kupitia mikataba,” alisema Waziri Mkuu, Majaliwa.
Alisema hata hivyo hakuna ubaya, endapo wabunge watapendekeza kuwasilisha bungeni mikataba ya kiwango au aina fulani ili ijadiliwe na wabunge kwa niaba ya wananchi ili kulinda maslahi mapana ya taifa.
Kuhusu ufisadi katika mikataba, Waziri Mkuu alisema pamoja na mikataba kupitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pale inapobainika kuwepo kwa ukiukaji wa maadili na sheria za nchi, hatua mbalimbali zimekuwa zinachukuliwa kwa wahusika wa suala hilo
0 comments:
Post a Comment