Search This Blog

Tuesday, May 3, 2016

PANYA ROAD WAVAMIA MSIBANI, WAOMBOLEZAJI WAPORWA MALI ZAO


KATIKA hali isiyo ya kawaida, vijana wa kihuni maarufu kama panya road, Jumatano iliyopita katika maeneo ya Mwananyamala kwa Kopa jijini Dar es salaam walivamia msibani na kuwaibia waombolezaji.

Mwandishi wetu aliyekuwa maeneo hayo, alikuta kijana mmoja akiwa ameuawa na watu wenye hasira kali na alipouliza sababu, aliambiwa kuwa alikuwa na vijana wenzake wapatao kumi ambapo waliwavamia watu waliokuwa msibani na kuwapora.
“Huyu marehemu ni panya road, alikuwa na wenzake wakawa wanawapora akina mama simu na mabegi msibani, huyu akadakwa na wananchi wenye hasira kali ambao walimwangushia kipigo hadi akapoteza maisha,” alisema shuhuda mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Said.
Alisema mara baada ya vijana hao kuvamia katika msiba huo, kulitokea vurumai kubwa na ikasababisha akina mama wengi kupoteza mali zao hasa simu na mabegi kwani yalikwapuliwa na wahalifu hao.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwa Kopa, Juma Mbilingu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Nichukue nafasi hii kuwaomba wazazi na hata wananchi wengine kuchukua jukumu la kuhakikisha familia zao hazizalishi panya road,” alisema na kuongeza kuwa hajui jina wala sehemu anayotoka kijana huyo aliyeuawa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (pichani) amekuwa akihimiza watu kufanya kazi badala ya kufanya mambo ya uhuni kama wanavyofanya panya road.

“Ninawaomba wazazi kuwaangalia watoto wao. Hawa vijana wanaofanya uhuni wana wazazi lakini haya ni matokeo ya kupewa malezi mabovu kutoka kwa wazazi wao.
Polisi waliitwa na kufika kisha kuchukua maiti ya kijana huyo na kuipeleka Hospitali ya Mwananyamala kuhifadhiwa.
Share:

0 comments:

Post a Comment