Search This Blog

Saturday, April 30, 2016

VINARA WA MADENI YA SERIKALI WATAJWA, POLISI YAONGOZA


Jeshi la Polisi limeibuka kinara miongoni mwa taasisi 91 za Serikali zilizolimbikiza madeni hadi kufikia Sh1.4 trilioni, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebainisha.
Ripoti hiyo ya hesabu zinazoishia Juni 30, mwaka jana, inasema jeshi hilo linaongoza kwa kudaiwa Sh385 bilioni likifuatiwa kwa mbali na Wizara ya Afya inayodaiwa Sh180.8 bilioni.
Kauli ya CAG
CAG, Profesa Mussa Juma Asaad anasema: “Sehemu kubwa ya deni ni kutoka Jeshi la Polisi ambalo ni sawa na asilimia 27 ya jumla ya deni lote; ya pili ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikiwa na asilimia 13 na Wizara ya Maji asilimia 10 ya deni lote.”
CAG anasema jumla ya madeni hayo imeongezeka mara mbili kutoka Sh772.5 ya mwaka uliotangulia hadi Sh1.4 trilioni sasa. “Kumekuwapo na ongezeko kubwa la madeni kiasi cha Sh671,350,983,378.30 sawa na ongezeko la asilimia 89,” anasema CAG katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni.
“Mwenendo wa deni, kwa kipindi cha miaka miwili, utaathiri utekelezaji wa mipango ya Serikali. Hii ni kwa sababu, badala ya kutekeleza mipango iliyopo, itakuwa inalipa madeni ya miaka ya nyuma,” inasema taarifa hiyo.
CAG anaongeza kuwa ongezeko kubwa la deni bila ya kuonyesha juhudi za kulilipa linavuruga uhusiano mzuri uliokuwapo kati ya wizara, wakala, idara na sekretarieti za mikoa pamoja na watoa huduma wake na watumishi; na huweza kusababisha utoaji wa huduma usioridhisha kwa umma.”
Anasema taasisi hizo zinaweza kushtakiwa kwa kosa la kushindwa kulipa deni kwa wakati hivyo: “Ninapendekeza kwa Serikali kuhakikisha fedha zinatolewa kama zilivyoidhinishwa na kupitishwa na Bunge ili kupunguza limbikizo kubwa la deni ambalo linaweza kusababisha hatari ya kudaiwa na kupunguza uaminifu, kuingiza katika bajeti ya mwaka ufuatao madeni yote ili kuepuka mgogoro na watoa huduma na wadau wengine.”
Pia, anaitaka Serikali kupitia upya mchakato wa maandalizi ya bajeti ili kuhakikisha ile inayoandaliwa inaendana na shughuli zilizopangwa na mahitaji yote kwa ujumla.

Kitwanga asema hajui
Alipoulizwa, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema hafahamu lolote na hawezi kuzungumzia suala hilo badala yake aulizwe Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Projest Rwegasira ambaye hata hivyo, hakupatikana alipopigiwa simu.
“... Hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa, mtafute Katibu Mkuu atakupa majibu,” alisema Waziri Kitwanga.

Ummy na deni la MSD
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kwa sasa watahakikisha wanapata fedha kutoka Hazina ili kumaliza madeni hayo hasa yale ambayo ni ya mikataba ya huduma zilizokwishatolewa.
“Mfano deni la MSD la zaidi ya Sh120 bilioni ambalo kati yake Sh67 bilioni zimehakikiwa na CAG, tumetenga fedha katika bajeti ijayo kulilipa,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali sasa imefuta huduma ya chakula kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya Serikali vya uuguzi na utabibu, hivyo wanafunzi wanatakiwa kujigharamia.
Kuhusu wagonjwa wanaotibiwa nje ya nchi, alisema Serikali itawapunguza na kujenga uwezo kwa hospitali za ndani.
“Hivi sasa deni ni zaidi ya Sh28 bilioni, hivyo tumedhamiria kujikita katika kujenga uwezo wa ndani kwa kusimika vifaatiba vya kisasa,” alisema.

Simbachawene: Sababu ni siasa
Waziri Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema madeni hayo yanatokana na mashinikizo ya kisiasa ya kutaka fedha zilizopangwa kufanya miradi mbalimbali kuhamishiwa katika matumizi mengine.
“Mfano, hili suala la Katiba Mpya, kuna fedha zilitengwa kwa ajili ya shughuli nyingine katika halmashauri lakini kutokana na wapinzani kushinikiza Katiba Mpya wakati mtizamo ulikuwa kuirekebisha iliyopo, baadhi ya fedha zilipelekwa kwenye mchakato wa kuipata Katiba hiyo,” alisema Simbachawene.
Alisema zipo fedha ambazo zilitengwa kwa ajili ya matumizi muhimu katika halmashauri lakini zilipelekwa katika Uchaguzi Mkuu kwa sababu tu ya mashinikizo ya kisiasa ambayo wakati mwingine yanakuwa hayana msingi.

Dk Mahiga anatafiti
Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga alisema bado anawasiliana na wataalamu wake kujua sababu ya kuwapo kwa deni hilo katika wizara yake.
“Jana tu nimewaagiza wataalamu wangu waniletee taarifa ya madeni ya wizara, nadhani tuwasiliane kuanzia kesho nitaweza kueleza mikakati ya kulipa. Ni kweli tumepata hati safi ya CAG, lakini hayo madeni bado sijayajua,” alisema Dk Mahiga.

Taasisi nyingine
Taasisi iliyoshika nafasi ya tatu kwa madeni ni Wizara ya Maji inayodaiwa Sh150.5 bilioni ikifuatiwa na Wizara ya Ujenzi (Sh135.7 bilioni), Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) inayodaiwa Sh93.2 bilioni na Jeshi la Wananchi wa Tanzania – JWTZ (Sh91.5 bilioni).
Nyingine ni Jeshi la Kujenga Taifa – JKT (Sh67.9 bilioni), Jeshi la Magereza (Sh59.2 bilioni) Hazina (Sh38.5 bilioni) na nafasi ya 10 imechukuliwa na Wizara ya Mambo ya Nje inayodaiwa Sh21.1 bilioni.
Taasisi yenye madeni kidogo iliyoshika nafasi ya 91 katika orodha hiyo ni Ubalozi wa Tanzania, Lilongwe, Malawi unaodaiwa Sh14, 292,697.

Vielelezo vya deni
Katika ripoti yake, CAG amefichua kuwapo kwa taasisi tatu za Serikali ambazo hazikuonyesha viambatanisho vya malipo yanayofikia Sh23.3 bilioni yanayotokana na huduma kutoka kwa wazabuni mbalimbali.
“Taasisi husika zilishindwa kuthibitisha uhalali wa madai hayo baada ya kushindwa kuwasilisha viambatisho na nyaraka za uhalali wake. Maofisa masuuli wanaohusika waweke mifumo ya udhibiti iliyo madhubuti ili kuhakikisha madai yote kwenye taarifa ya fedha yanakuwa na nyaraka zinazothibitisha huduma iliyotolewa,” anasema.
Taasisi hizo ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (Sh3.2 bilioni), Wizara ya Mambo ya Ndani (Sh1.8 bilioni) na Wizara ya Afya (Sh18.3 bilioni).
Share:

BAADA YA MAFUTA UGANDA-TZ, NI GESI TZ-UGANDA


Baada ya Tanzania na Uganda kukubaliana mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta utekelezwe kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, matumaini mengine mapya yameonekana kutokana na Uganda kuweka wazi azma yake ya kujenga bomba jingine la gesi katika njia hiyohiyo kwa ajili ya biashara na Tanzania.

Licha ya kutofafanua kwa kina juu ya mpango huo, Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Serikali ya Uganda na Tanzania bado ziko kwenye majadiliano ya kuanzisha mradi mwingine wa bomba hilo la gesi.

“Ni mpango mpya bado tunajadiliana, kuna uwezekano mkubwa wa kujenga bomba hilo lakini utekelezaji wake utaanza baada ya mradi huo wa bomba la mafuta wa sasa kukamilika,” alisema.

Waziri Muloni aliyekuwa ameongozana na mwenyeji wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kwanza wa jopo la watalaamu wa sekta mbalimbali waliokutana kwa mara ya kwanza kuandaa mpango wa utekelezaji wa mradi huo.

Mkutano huo unafanyika ikiwa ni siku sita tangu azungumze na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili nchini akitokea Kampala ambako Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alitangaza kuwa bomba hilo la mafuta ghafi kutoka Hoima, Ziwa Albert litapita katika ardhi ya Tanzania kwenda Bandari ya Tanga.

Waziri Muhongo alisema mbali na bomba hilo, nchi nyingine za Afrika Mashariki pia zimekubali kununua gesi ya Tanzania.

Kuhusu mradi wa bomba, Profesa Muhongo alisema nchi hizo zimekubaliana kukamilisha Kazi hiyo kabla ya makubaliano ya awali ya 2020.

Makubaliano mengine ya nchi hizo ni kuchangia ujenzi wa mtambo wa kuchakata mafuta ghafi utakaojengwa Uganda ambao alisema utasaidia kuweka akiba ya mafuta kwa ajili ya biashara kwa nchi wanachama.  
Share:

SAFARI YA DAWA MIAKA MINNE, MSD YAJITETEA


Bohari ya Dawa (MSD) imetoa ufafanuzi kuhusu dawa za sh.bilioni mbili kuwa njiani kutoka Bohari ya Dawa ya Keko kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu mwaka 2012.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema hakuna dawa ambazo ziko njiani tangu mwaka 2012 kutoka Bohari ya Dawa kwenda Muhimbili kama ilivyodaiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bungeni.

Bwanakunu alisema kuwa ripoti ya CAG ilionesha dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya sh.bilioni 2.03 havikuwa vimefika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tangu Mei 2012 licha ya kuonekana kwenye ankara 23 na Bohari ya Dawa.

"Tunapenda kutoa ufafanuzi kuwa ankara hizo sio kwamba dawa hazikufika hospitalini hapo, bali hazikuonekana kwenye vitabu vya kupokelea mali vya Hospitali ya Muhimbili" alisema Bwanakunu.

Alisema kwamba baada ya kupitia nyaraka zake, Bohari ya Dawa mpaka sasa imefanikiwa kupata uthibitisho wa hati za kupelekea mali za dawa na vifaa tiba vyote vilivyopokelewa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambavyo ni pamoja na dawa za figo na moyo ambazo zilikwishapelekwa Muhimbili.

Aliongeza kuwa pamoja na juhudi za MSD imewasiliana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuainisha taarifa za kwenye ankara na shehena ya dawa na vifaa tiba vilivyopelekwa hospitalini hapo kwani utaratibu wa kupeleka na kukabidhi dawa hospitalini unamlazimu mpokeaji kusaini ankara ya kupeleka mali ambazo zote zipo MSD.

Akitolea ufafanuzi kuhusu picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii za gari aina ya lori lenye herufi "MSD" na kutoa maelezo kuwa ni gari la MSD amesema nembo inayoonekana kwenye gari hilo siyo ya Bohari ya Dawa.

Katika ripoti ya CAG ilionesha kwamba madawa na vifaa tiba ambavyo havikupokelewa kwa muda mrefu kutoka MSD vilikuwa vyenye thamani ya sh.bilioni 2.03 ambapo katika hali ya haikutajiwa kuchukua zaidi ya wiki moja kufikishwa sehemu husika ukizingatia ofisi zao ziko Dar es Salaam.
Share:

WAHUSIKA WA ESCROW NA HATIFUNGANI YA STANDARD BANK KUSHTAKIWA


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imepokea ushauri uliotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) wa kuishitaki Benki ya Standard (ICBC) ya Uingereza, kuhusu ufisadi uliofanyika katika mkopo wa Dola za Marekani milioni 600 (Sh trilioni 1.2) ambazo Serikali ilikopa kwa kutumia hati fungani.
Ushauri mwingine uliotolewa na Zitto ambao Waziri Mkuu amesema Serikali itaufanyia kazi ni kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwafikisha mahakamani wahusika wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, ili sheria ichukue mkondo wake.
Zitto alitoa ushauri huo bungeni mjini hapa juzi, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, iliyowasilishwa na Waziri Angela Kairuki.
Hotuba ya bajeti ya ofisi hiyo inajadiliwa na wabunge pamoja na ile ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyowasilishwa na Waziri wake, George Simbachawene.
Akizungumza na wanahabari jana, Waziri Mkuu alisema, hoja ya Zitto ina mashiko na akiwa msimamizi wa shughuli za Serikali bungeni, atahakikisha ushauri huo unafanyiwa kazi. “Sisi kama Serikali tutaifanyia kazi na pale tutakapoona tumefikia katika hatua ya kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ushauri huo, tutafanya hivyo,” alisema.
Benki ya Standard Kuhusu Benki ya Standard ya Uingereza, Zitto alisema mkopo huo wenye riba yenye kuweza kupanda na kushuka, umeanza kulipwa Machi mwaka huu na utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa inayolingana.
Alisema, ifikapo mwaka 2020, Tanzania itakuwa imelipa deni hilo pamoja na riba ambayo ni Dola za Marekani milioni 897 sawa na Sh trilioni 2, huku akidai kuwa mkopo huo umegubikwa na ufisadi na wapo baadhi ya Watanzania wamefikishwa mahakamani kuhusu sehemu ya mkopo huo.
Alisema Takukuru katika kesi hiyo, inasaidiwa na wataalamu kutoka Uingereza katika kesi inayohusu Benki ya Uingereza, huku kukiwa na Watanzania walioandika ‘petition’ kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wakitaka ukweli wote kujulikana.
Escrow Kuhusu IPTL Tegeta Escrow, Zitto alisema mwaka 2014, Takukuru iliijulisha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwamba ilikuwa inachunguza na kumaliza uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya Stanbc Tanzania.
Alisema katika taarifa zote ambazo Takukuru inatoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna mahali inapozungumzia maendeleo ya suala hilo.
Share:

TANI 24 ZA SUKARI ILIYOFICHWA ZANASWA SINGIDA


KAULI ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwa baadhi ya wafanyabiashara wameficha sukari ili kutengeneza uhaba sokoni utakaopandisha bei ya bidhaa hiyo, imedhihirika baada ya baadhi ya wafanyabiashara hao kuanza kukamatwa wakiwa na vidhibiti.
Kutokana na hali hiyo iliyosababisha bei ya bidhaa hiyo kuanza kupanda, Waziri Mkuu Majaliwa, alitangaza uamuzi wa Serikali kuagiza sukari yake nje itakayouzwa kwa bei elekezi kwa wananchi ya Sh 1,800 kwa kilo, ili kuzuia ongezeko hilo haramu la bei.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Amanzi alitangaza polisi kuwashikilia wafanyabiashara wawili wa mjini hapa kwa tuhuma za kukutwa na zaidi ya mifuko 655 ya sukari, sawa na tani 24.3, ikiwa imekifichwa kwenye stoo zao.
Kwa mujibu wa Amanzi, wafanyabiashara hao walikamatwa kwenye msako ulioendeshwa na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa Singida pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Amanzi alisema kuwa msako huo uliendeshwa baada ya kupata taarifa za siri kuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wameficha sukari, ili waje kuiuza kwa bei ya juu kwa wateja wao kwa kisingizio kuwa kuna uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo.
“Katika msako huo, tumemnasa Mohamed Alute Ally (44), mfanyabiashara wa eneo la Unyankindi aliyekutwa na mifuko 335 ya kilo 25 kila mmoja na Yusufu Suleiman (39), mfanyabiashara wa eneo la Minga katika manispaa ya Singida aliyepatikana na mifuko 320 ya kilo 50,” alisema.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa mwito kwa wafanyabiashara wote kuacha kuficha bidhaa zote muhimu, ikiwemo sukari na mchele, bali waiuze kwa bei halali kwa wateja wao. Wakati huo huo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Joseph Mchina, amesema msako mkali unaohusisha kikosi kazi maalumu pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama utaendelea kwa nguvu zote na kusisitiza kuwa kuhodhi bidhaa kwa sababu yoyote ile ni kosa la uhujumu uchumi.
Mmoja wa Wakala wa Kiwanda cha Sukari cha TPC Moshi Mjini, Salim Nagji, amesema mfuko mmoja wa sukari huuzwa Sh 92,650 lakini tangu sukari iadimike mfuko unauzwa kati ya Sh 115,000 na Sh 120,000 huku kilo moja ikiuzwa kati ya Sh 2,400 na Sh 2,800 kwa kilo kinyume na bei elekezi ya Sh 1,800.
Share:

TANI 105 ZA PEMBE ZA NDOVU NA FARU KENYA KUTEKETEZWA MBELE YA RAIS KENYATTA

Elfenbeinverbrennung in Kenia
Kenya inajitayarisha kuchoma moto tani 105 za pembe za ndovu na faru leo Jumamosi (30.04.2016), ambapo Leonardo DiCaprio na Elton John watakuwa miongoni mwa watu watakaohudhuria tukio hilo.
Kiasi cha tani 105 za pembe za ndovu zitakazochomwa moto nchini Kenya
Kenya itachoma tani 105 za pembe za ndovu na zaidi ya tani moja ya pembe za faru leo Jumamosi (30.04.2016) ikiwa sehemu ya kupambana na majangili.
Leonardo DiCaprio na Elton John ni miongoni mwa watu mashuhuri watakaoshuhudia lundo la pembe za ndovu likichomwa moto wakati wa tukio hilo la kwanza la aina yake tangu mwaka 1989.
Elfenbeinverbrennung in Kenia
Mmoja kati ya walinzi wa wanyama pori nchini Kenya akipanga pembe hizo
Kwa mujibu wa wakfu wa wanyama pori barani Afrika AWF, kiasi cha pembe za ndovu 35,000 wameuwawa katika bara la Afrika mwaka jana, kutoka jumla ya tembo 500,000.
Hali ni mbaya zaidi kwa faru. Tangu mwaka 1960, karibu asilimia 98 ya faru weusi wa Afrika, wameuwawa.
Biashara haramu
Kilo moja ya pembe ya ndovu inaripotiwa na shirika linalopigania ulinzi wa wanyamapori kuwa ina thamani ya dola 1,100 katika soko la chini kwa chini, wakati pembe ya faru inakwenda mara 50 zaidi ya kiasi hicho, na China ikiwa ndio soko kuu.
Thailand Zoll beschlagnahmt 3 Tonnen Elefantenstoßzähne
Pembe za ndovu zikipangwa
Mashirika ya ulinzi wa mazingira yameeleza kuunga kwao mkono kuharibiwa kwa shehena hiyo. "Kuhifadhi pembe hizo zilizokamatwa ni kazi kubwa na yenye gharama kubwa," amesema Daniela Freyer kutoka shirika la Pro Wildlife.
Pia kuna hatari, wakati mataifa masikini yanaweza kupata fedha nyingi kwa kujiingiza katika biashara haramu ya pembe za ndovu.
Serikali ya Kenya kwa muda mrefu ilikuwa inataka kupigwa marufuku biashara hiyo duniani, wazo litakalojadiliwa tena katika mkutano wa shirika la CITES ambao unaanza mjini Johannesburg mwishoni mwa mwezi Septemba.
Deutschland Uhuru Kenyatta in Berlin
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta
Nchi nyingi zimepiga marufuku biashara ya pembe za ndovu katika miaka ya 1980, lakini kuna tofauti, wakati China na Japan zinaruhusu kununua pembe hizo kutokana na kulegezwa kwa vizuwizi, Freyer amesema.
Wanastahili maisha zaidi
Mamlaka ya hifadhi ya mali asili nchini Kenya imelitangaza tukio la leo Jumamosi katika ukurasa wa Twitter chini ya hashtag: "worthmorealive" wanastahili maisha zaidi.
Dai hilo hakika ni la kweli kwa ajili ya nchi hiyo ya Afrika mashariki ambayo ni maarufu kwa utalii, ambayo imejipatia kiasi ya dola bilioni 2.2 ama kiasi ya asilimia 4 ya pato jumla la taifa kutokana na utalii mwaka jana, kwa mujibu wa shirika la utalii la dunia.
Großbritanien BAFTA 2016 Leonardo DiCaprio
Mcheza sinema Leonardo DiCaprio atakuwapo katika tukio hilo nchini Kenya.
Zaidi ya asilimia 9 ya wakaazi milioni 46 nchini Kenya wanafanyakazi katika sekta hiyo, wakati idadi inaongezeka kila mwaka. Watalii wanavitiwa nchini humo na maili kadhaa za fukwe nzuri katika bahari ya Hindi na mbuga za wanyama ndani ya nchi hiyo.
Gavin Shire kutoka kitengo cha samaki na wanyamapori nchini Marekani FWS amesema kwamba maafisa wa Kenya wanahitajika kuhakikisha kwamba pembe hizo zinaharibiwa katika njia ambayo inafanya soko haramu la pembe hizo linakuwa halifai.
Share:

JPM AIGUSIA LUGUMI KIAINA, AUITA 'MKATABA MBOVU'


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi nchini na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujirekebisha kwa kutekeleza wajibu wao huku wakitanguliza maslahi ya taifa.

Rais Magufuli ametoa maagizo hayo jana tarehe 29 Aprili, 2016 wakati akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa polisi wa mikoa, Mawakili wafawidhi wa serikali wa Mikoa na Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na Vikosi, kinachofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Mikutano wa Dodoma uliopo katika eneo la Tambukareli Mjini Dodoma.

Awali kabla ya kutoa hotuba yake Rais Magufuli aliwapa nafasi Makamanda na Mawakili Wafawidhi hao kutoa maoni yao juu ya changamoto zinazowakabili katika kutekeleza wajibu wa kufanya upepelezi na kuendesha mashitaka, hususani kujua sababu za kuchelewesha kesi za makosa ya jinai, ambapo wamedai ufinyu wa bajeti ndio sababu kubwa ya kucheleweshwa kwa kesi za hizo.

Kufuatia kutajwa kwa changamoto hiyo Rais Magufuli ameahidi kuhakikisha anawatafutia fedha kwa ajili ya kukabiliana nazo, lakini ametaka fedha zitakazotafutwa zitumike vizuri kwa kuwa taarifa zinaonesha Jeshi la Polisi limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake wa kazi.

Ametolea mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kununulia vifaa na sare za askari, ama mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya Polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.

"Oysterbay pale ni eneo ambalo ni very prime, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua nyinyi, akapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa. Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale, mkaweka investment na Polisi wenu wakakaa pale. Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia vibaya nikimaliza mkutano huu, nataka muelewe na muelewe ukweli direction ninayoitaka mimi" Amesema Rais Magufuli

Aidha, Rais Magufuli ameitaka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka kujipanga kufanya kazi kwa ufanisi na ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya serikali kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya kuwa na wanasheria mahiri.

"Niwaombe mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi mtangulize maslai ya nchi mbele, kwa sababu kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili wachache, nasema wachache, panapokuwa na kesi inayohusiana na pesa pesa, wana misemo yao wanasema dili limepatikana, na saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani wana-collude Mawakili wa serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu, na wanapo-collude siku zote serikali inashindwa. Unapoona hali hiyo ya kila siku serikali inashindwa, halafu siku hiyo unataka serikali ikuwezeshe, kwa vyovyote serikali inapata kigugumizi" amesisitiza Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli pia amelitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maafisa wa Polisi kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa wahalifu wa ujambazi.

Hata hivyo Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kwa kazi kubwa wanayoifanya na ametaka apelekewe mpango wa mahitaji yao ili atafute namna ya kuimarisha vyombo hivyo.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma
29 Aprili, 2016
Share:

Friday, April 29, 2016

TRUMP AIKUMBUKA TZ YA 1998, AKOSEA KUITAMKA


Mgombea urais wa chama cha Republican Donald Trump amekejeliwa mtandaoni baada ya kuonekana akiboronga akitamka Tanzania wakati wa kutoa hotuba.
Bw Trump alikuwa akizungumzia mashambulio ya kigaidi yaliyotekelezwa katika mabalozi ya Marekani nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998 wakati wa kuzungumzia sera yake ya kigeni.
Badala ya kutamka vyema ‘Tanzania’ anasikika akitamka ‘Tan-zay-nia’.
Mashambulio hayo yalitekelezwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda.
Msemaji wa ikulu ya White House pia alimcheka Bw Trump alipoulizwa kuhusu vile mfanyabiashara huyo tajiri kutoka New York alivyotamka jina Tanzania.
“Kweli, yamkini jinsi ya kutamka huwa haijaelezwa kwenye kifaa cha kuonesha maandishi ya hotuba,” alieleza afisa wa habari wa ikulu Bw Josh Earnest.
Wakati wa hotuba hiyo, alizungumzia pia kuhusu kundi la Islamic State ambalo kwa sasa limeanza kunawiri nchini Libya. Kundi hilo hujulikana pia kama Isis.
“Na sasa Isis wanapata mamilioni na mamilioni ya dola kila wiki kwa kuuza mafuta ya Libya. Na wajua? Huwa hatuwawekei vikwazo vya kutouza, hatuwaangushiwi mabomu, hatufanyi lolote,” alisema.
“Ni kana kwamba nchi yetu haifahamu yanayofanyika, jambo ambalo huenda likawa kweli.”
Kwenye hotuba yake, Bw Trump alikosoa sera za kigeni za Rais Barack Obama.
Lakini Bw Earnest alipuuzilia mbali madai ya Bw Trump ambaye kwa sasa anaongoza miongoni mwa wagombea wanaotaka kupeperusha bendera ya chama cha Republican.
Share:

ZUMA KUJIBU MASHTAKA 800 KORTINI


Mahakama kuu Afrika kusini imeruhusu kuangaliwa upya uamuzi uliopitishwa 2009 wa kutupilia mbalia mashtaka yote ya ufisadi dhidi ya rais Jacob Zuma.
Majaji wamesema kaimu mkurugenzi wa upande wa mashtaka alichukuwa hatua kwa wepesi ya kuondosha mashtaka takriban 800 dhidi ya Zuma.
Mwendesha mashtaka ametetea uamuzi huo kwa misingi kuwa serikali iliingilia kati kesi hiyo, inayohusu makubaliano ya biashara ya silaha zenye thamani za mabilioni ya dola.
Lakini mahakama kuu imesema upande wa mashtaka unaonekana kuwa ulikuwa tayari kuendelea na kesi hadi usiku wa kuamkia kuwasilishwa tangazo hilo, hatua iliyotoa nafasi kwa Zuma kuwania urais.
Ushahidi umetokana na 'kanda za kijasusi'  ambazo ni mazungumzo ya simu yalionakiliwa kati ya aliyekuwa jasusi wa Afrika kusini na aliyekuwa mwendesha mashtaka mkuu, ambapo wanasikika wakipanga kumzuia Zuma kuwania urais nchini humo.
kwa miaka mingi upinzaniumetaka upewe kanda hizo ukidai kuwa ushahidi wa rushwa huenda ukawa pia uko kwenye kanda hizo.
Upinzani kwa mara nyengine umetaka rais Jacob Zuma ajiuzulu,abaye tayari yumo kwenye shinikizo baada ya kupatikana kukiuka katiba kwa kutozingatia matokeo yaliofichuliwa na taasii ya serikali.
Share:

KAMA ULIPITWA, HII NDIYO HOTUBA YA MH.ZITTO KABWE ILIYOIBUA HOJA NA KASHFA MBALIMBALI BUNGENI


Mchango wa Ndg. Zitto Kabwe Bungeni, Tarehe 28 Aprili 2016
Ofisi ya Rais Utawala Bora
Ukiukwaji wa Sheria ya Bajeti
Mheshimiwa Spika, Tangu tuanze Mkutano huu wa Bajeti mwaka 2016 kumekuwa na malalamiko kutoka kwa Wabunge na hasa wabunge wa kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu ukiukwaji wa Sheria mbalimbali za nchi katika masuala ya Bajeti. Jana jioni Mwenyekiti wa Bunge Mheshimiwa Andrew Chenge alitoa Changamoto kuwa Wabunge tuseme ni sharia gani zimekiukwa katika mchakato mzima wa Bajeti ya Nchi hivi sasa. Kwa maoni yangu, kuna ukiukwaji kadhaa wa sharia ya Bajeti, sharia namba 11 ya mwaka 2015 katika mchakato wa Bajeti ya Mwaka huu. Nitaeleza kwa ufupi.
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 8 cha sheria ya Bajeti kinaeleza namna ambavyo mfumo wa Bajeti ya Serikali unapaswa kuwa. Vifungu cha 8(1)(b) na 9(1)(a) na 19(1) vinaeleza namna mchakato wa Bajeti unavyopaswa kuwa. Vifungu hivi vinataka “Planning and Budget Guidelines” zipitishwe na Bunge katika mkutano wake wa Mwezi Februari kila mwaka. Sheria inataka “budget ceilings” ziidhinishwe na Kamati ya Bajeti na baadaye Bunge linapokaa kama Kamati ya Mipango.
Mheshimiwa Spika, Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango na kupitisha Mpango wa Bajeti uliokuwa na Bajeti ya Tshs 23.7 trilioni kama ulivyowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango. Hata hivyo Bajeti inayojadiliwa sasa ni Tshs 29.5 trilioni tofauti kabisa na sio tu viwango vilivyopitishwa na Bunge mwezi Februari bali pia hata vipaumbele vyake ni tofauti. Hili ni suala la Utawala bora (governance issue) kwani taratibu za utungaji wa Bajeti zimeainishwa na sheria na kama sheria hazifuatwi ni vigumu sana hata Bajeti yenyewe kutekelezwa. Ili kurekebisha hali hii ni lazima Bunge likae tena kama kamati ya Mipango na kupitisha upya viwango vya juu vya bajeti kabla ya mjadala wa Bajeti kuendelea au angalau kabla ya kupitisha Bajeti Kuu mwezi wa Juni 2016.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais Ikulu inapasa kuzingatia sana sheria na taratibu tulizojiwekea kwani madhara ya kutofuata sheria ni makubwa mno. Kwa mfano hivi sasa Bajeti za Taasisi hazimo kwenye vitabu vya Bajeti ya Serikali kinyume na Sheria ya Bajeti ambapo hivi sasa Bajeti za Taasisi zote za Umma zinakuwa ni sehemu ya Bajeti ya Serikali na Wabunge wanapaswa kuwa na nyaraka za bajeti hizo. Ofisi ya TR kwa mujibu wa kifungu cha 17(a) cha Sheria ya Bajeti ilipaswa kuunganisha Bajeti za Mashirika yote ya Umma na kutoa kitabu chake kwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, Serikali inapaswa kutoa maelezo ya kina kwa Wabunge kuhusu masuala haya ili kuzuia ukiukwaji wa Sheria tulizojitungia wenyewe.
TAKUKURU na kesi za Ufisadi Mkubwa Nchini
1. Ufisadi wa HatiFungani ya Tshs 1.2 trilioni Standard Bank ya Uingereza
Mheshimiwa Spika, Tarehe 8 Machi mwaka 2013 Serikali ya Tanzania ilikopa fedha $600 milioni ( 1.2 trilioni) kutoka nje kwa msaada wa Benki ya Standard ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank ICIC Plc. Mkopo huo wenye riba yenye kuweza kupanda (floating rate) umeanza kulipwa mwezi Machi mwaka huu ( kama Serikali imeanza kutekeleza mkataba). Mkopo huu utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo 9 inayolingana. Ifikapo mwaka 2020, Tanzania italipa deni pamoja na riba jumla ya $897 milioni ( takribani tshs 2 trilioni ). Mkopo huu umegubikwa na ufisadi na kwa kuwa baadhi ya Watanzania wamefikishwa mahakamani kuhusiana na sehemu ya mkopo huu, sitapenda kueleza upande wa waliopo mahakamani. Kesi iliyopo mahakamani inahusu $6 milioni ambazo inasemekana ( kwa mujibu wa nyaraka za mahakama) kuwa zilitumika kuhonga maafisa wa Serikali ili Benki hiyo ya Uingereza iweze kupata biashara iliyopata. Jambo la kushangaza ni kwamba wanaosemekana kula rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Vile vile waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Waliopo mahakamani ni wanaosemekena kutumika kupeleka rushwa. Mjumbe kashtakiwa, lakini aliyemtuma hajashtakiwa na aliyepelekewa kilichotumwa hajashtakiwa. Hapa kuna tatizo la msingi ambalo tukilitatua Serikali yetu itaepuka masuala kama haya siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, Hapa mbele yangu nina barua ambayo kundi la Watanzania zaidi ya 2000 kutoka kona zote za dunia wamesaini kutaka Benki ya Standard ya Uingereza ichunguzwe kwenye suala hili la HatiFungani. TAKUKURU walitumia taarifa ya Taasisi ya Uingereza ya SFO katika kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hili. SFO haikufanya uchunguzi dhidi ya Benki ya Uingereza ya Standard Bank. Hatujui ni kwa maslahi mapana ya Uingereza au ni kwa kupitiwa. Sisi Tanzania tumejikuta tunafuata matakwa ya Uingereza katika jambo hili, kiasi cha hata kutumia ushauri wa kitaalamu wa Waingereza katika jambo hili. Leo hii TAKUKURU inasaidiwa katika kesi hii na wataalamu kutoka Uingereza katika kesi inayohusu Benki ya Uingereza! Watanzania walioandika petition kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wanataka ukweli wote kujulikana – Standard Bank walihusika kwa kiwango gani katika kutoa rushwa ili kupata biashara? TAKUKURU wanapaswa kufanyia kazi jambo hili kwa kuwafungulia mashtaka Standard Bank, mashtaka ya kutoa rushwa ili kupata biashara nchini. Hata hivyo TAKUKURU inaogopa wazungu, inaogopa kuwaudhi watu wanaowapa ushauri wa kitaalamu kuhusu kesi za rushwa!
Mheshimiwa Spika, maslahi ya Tanzania hapa ni makubwa mno. Iwapo tutafanikiwa kuonyesha kuwa Benki ya Standard ilihonga kupata biashara nchini kwetu Tanzania itafaidika kwa namna mbili. Moja, itakuwa ni fundisho kubwa kwa makampuni ya kimataifa kwamba Afrika sio mahala pa kuhonga na kupata kazi na kutoadhibiwa. Mbili, Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake. Tutakuwa tumeokoa zaidi ya tshs 2 trilioni katika Deni la Taifa na kuelekeza fedha tulizokuwa tulipe riba kwenda kwenye kuhudumia wananchi wetu kwenye Afya na Elimu. TAKUKURU waongozwe na maslahi mapana kwa Taifa badala ya kutafuta sifa ndogo ndogo za ‘wangapi wamefikishwa mahakamani’. Ni lazima taasisi zetu sasa zianze kutazama mambo kwa picha kubwa.
Mheshimiwa Spika, hii sio mara ya kwanza SFO kufanya ilichofanya dhidi ya Tanzania. Mnakumbuka kesi ya rada na Shirika la BAE la Uingereza. Safari hii Tanzania isikubali kubeba tu makubaliano ambayo SFO inafanya na makampuni ya kimataifa. Ni lazima tufanye uchunguzi wetu na tufungue kesi dhidi ya makampuni haya. Haiwezekani wawe ni Watanzania tu wanaoshtakiwa kwa rushwa na kuwaacha wanaotoa rushwa hizo wakiendelea na biashara zao kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, Taarifa zilizopo sasa kwenye vyombo vya habari ni kwamba Benki hii kupitia tawi lake la Tanzania ( Stanbic Bank ) siku ambayo walipata ‘deal’ la Bond ndio siku hiyo hiyo walipewa kazi na Serikali ya kufungua akaunti ya Escrow kuhusu fedha za Bomba la Gesi kutoka Mtwara. Kimsingi biashara hii ya Escrow akaunti katika Benki hii ni kubwa zaidi kutoka ile ya mkopo kwani ni biashara ya kutunza fedha za Bomba kwa miaka 20! Benki hii ilipata biashara kubwa kama hii bila ya kuwepo kwa zabuni yeyote ile na kuleta ushindani. Lakini pia kama kulikuwa na umuhimu wa kufungua akaunti hii ni kwanini Shirika la TPDC halikufungua akaunti hii katika Benki Kuu ya Tanzania? Haya ndio mambo TAKUKURU wanapaswa kuchunguza katika kulinda maslahi ya nchi yetu dhidi ya makampuni makubwa kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, Vile vile kuna taarifa kwamba hata fedha ambazo zilipatikana kutokana na mkopo huu hazikufika kule kunakotakiwa. Nimewasilisha maswali Wizara ya Fedha kutaka kujua miradi ambayo fedha hizi zilikwenda. Hata hivyo kutokana na orodha ya miradi niliyonayo na kutokana na habari za hivi karibuni za Serikali kudaiwa na wakandarasi, mradi wa Kinyerezi na hata mradi wa Kiwira, ni dhahiri kuwa sehemu ya fedha zilizopatikana katika mkopo huu hazikupelekwa huko. Uchunguzi wa kina unatakiwa kwenye eneo hili ili kupata ukweli na kuzuia mambo kama haya kutokea siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, nitatumia kanuni ya 120(2) kutaka Bunge tako tukufu kuunda Kamati Teule kuichunguza Benki ya Standard ICBC ya Uingereza na kampuni yake dada ya Stanbic Tanzania kuhusiana na Mkopo wa Hatifungani $600m, matumizi ya mkopo huo na ufunguzi wa Akaunti ya Escrow ya Bomba la Gesi la Mtwara – Dar es Salaam. Kwa sasa ninawasilisha mezani nyaraka zote nilizonazo kuhusiana na Mkopo huu kwa ajili ya Bunge kupitia kabla ya kuwasilisha Hoja ya Kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuichunguza Standard Bank ICBC na Stanbic Tanzania
2. Uchunguzi wa IPTL Tegeta Escrow Account
Mheshimiwa Spika, Mwaka 2014 TAKUKURU waliijulisha Kamati ya Bunge ya PAC kwamba ilikuwa inachunguza na kumaliza uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya Stanbc Tanzania. Katika taarifa zote ambazo TAKUKURU inatoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna hata siku moja wanasema kuhusu uchunguzi huu na lini wahusika waliochota fedha za umma watafikishwa mahakamani. Naomba tupate kauli ya Serikali kuhusu jambo hili kwani ni moja ya JIPU kubwa ambalo tunadhani Serikali inalikimbia. Serikali inaogopa nini? Serikali inamwogopa nani? Kwanini kesi ya ufisadi wa IPTL unakaliwa kimya? Kwa maslahi ya nani?
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kigoma Mjini
Share:

UHABA WA SUKARI, SERIKALI YATENGA MADUKA MAALUM KAGERA


Serikali mkoani Kagera imesitisha uuzwaji wa sukari kwa biashara ya jumla, badala yake imetenga maduka maalumu kwa kila kata yatakayohusika kuwauzia wananchi sukari kwa bei elekezi ya Serikali,lengo likiwa ni kuondoa uhaba wa sukari na kuwaondolea kero wananchi.

Kwa mujibu wa Afisa Biashara mkoani hapa Isaya Tendega,uamuzi huo umefikiwa mara baada ya kubaini kuwa wapo baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya jumla wanaotumia changamoto ya upungufu wa sukari na kuiuza kwa bei ya juu tofauti na bei iliyoelekezwa na Serikali.

Tendega amesema kuwa hali ya Sukari iliyoko katika kiwanda cha kuzalisha Sukari cha Kagera ni yakutoshereza kwa wananchi wa mkoa wa Kagera,ingawa changamoto ya kuwepo uhaba wa Sukari inachangiwa kwa kiwango kikubwa kwa Wafanyabiashara kutoka nje ya mkoa kufika Bukoba kuchukua Sukari kwa bei yeyote wanayoitaka wao na kuufanya mkoa kukabiliwa na changamoto hiyo.

Amesema maduka maalumu husika yatakuwa yakisimamiwa na halmashauri za wilaya na Manispaa,hivyo kuwaomba wananchi wa mkoa wa Kagera,kuwa na uvumilivu kwa hatua ya utekelezaji huo inaendelea na kufikia Mei 2(Jumatatu)huduma ya maduka hayo itakuwa imeanza kuwahudumia wananchi.

Uhaba wa Sukari mkoani Kagera imekuwa changamoto kwa wananchi,hali inayosababisha wauzaji wa jumla kuuza sukari kwa bei ya 125,000/ huku bei ya rejareja ikiuzwa kati ya shilingi 2,400 hadi 2600/=huku lawama nyingi zikielekezwa kwa Serikali.
Share:

MAGUFULI ALITAKA JESHI LA POLISI LIJITATHMINI


Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania dkt John Pombe Magufuli amelitaka jeshi la polisi nchini kujitathimi kiutendaji kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu nchini ambapo wakati mwingine maafisa wa jeshi hili huusika.
Rais Magufuli amebainisha haya wakati wa kikao cha kazi na viongozi wa ngazi za juu wa jeshi la polisi kilichofanyika mkoani Dodoma.
Rais Magufuli pia amekemea vikali kukithiri kwa vitendo vya rushwa kwa baadhi yamaafisa wa polisi na mahakama akivitaja kuwa chanzo kikubwa cha kukua kwa uhalifu nchini.
Kwa upande mwingine Rais Magufuli amepinga vikali ubinafsishawaji wa eneo la kituo cha polisi la ostabay kutokana eneo hili kuwa bora zaidi katika kukabiliana na uhalifu jijini Dar es salaam
Kikao hiki kinakuja wakati jeshi la polisi nchini linakutana na wakati mgumu wa kupambana na uhalifu wa unaofanyika katika taasisi binafsi za fedha mkimwemo benki na maduka ya Mpesa.
Share:

MABADILIKO KAMATI ZA BUNGE, WABUNGE WANENA


Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya mabadiliko mengine ya kamati za Bunge kwa kuwaongeza wabunge wapya na kuwahamisha wengine kwenda kwenye kamati nyingine, jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wabunge wakidai linapunguza ufanisi.
Juzi, Spika Ndugai (pichani) aliwaongeza wabunge wanne wapya walioapishwa bungeni Aprili 19, kwenye kamati za Miundombinu; Ardhi, Maliasili na Utalii; Kilimo, Mifugo na Maji; na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Hayo ni mabadiliko ya pili tangu Bunge la 11 lianze rasmi vikao vyake katikati ya Novemba mwaka jana, ikiwa ni kipindi kifupi cha mabadiliko ikilinganishwa na Bunge la Tisa na 10.
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Bunge, mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa kanuni ya 116 (3) na (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2016, ili kuhakikisha kila mbunge anakuwa mjumbe wa kamati mojawapo ya Bunge. “Aidha, mabadiliko haya ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa kadri itakavyowezekana, Muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge unazingatia aina za wabunge kwa jinsia, pande za Muungano na Vyama vya Siasa vyenye uwakilishi bungeni, ujuzi maalumu, idadi ya wajumbe kwa kila kamati na matakwa ya wabunge wenyewe,” inasema taarifa hiyo.
Baadhi ya wabunge jana walipinga mabadiliko ya mara kwa mara ya wajumbe wa kamati, wakieleza kuwa hayaleti tija na uamuzi huo haufanywi kwa umakini.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisema mabadiliko hayo yanaonyesha namna ambavyo Spika Ndugai “anavyokosa umakini katika uundaji wa kamati hizo”.
“Spika hakuwa makini wakati anaziunda kamati hizo na sina jingine zaidi ya kusema, maana hilo liko wazi,” alisema Zitto.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha alisema uundaji wa kamati kila mara, unatokana na kiongozi huyo kutokuwa na umakini na mara nyingi anafanya kazi kwa shinikizo la vikao vya chama.
Msabaha alisema utaratibu wa kuvunja kamati na kuziunda unatokana na vikao vya wabunge wa CCM, ambavyo humshauri Spika juu ya nini kifanyike ili waweze kuubana upinzani, ushauri ambao anadai wakati mwingine unakosa tija.
Mbunge wa Sengerema William Ngeleja (CCM) alisema mabadiliko yanayofanywa hayana madhara yoyote, kwa kuwa ni jambo la kawaida kufanya maboresho na kuwataka wabunge kujifunza kupitia mchezo wa mpira ambao kila mtu anakuwa na namba yake, lakini uwanjani anacheza namba zote.
“Waangalie mfano wa Profesa Makame Mbarawa ambaye alipewa Wizara ya Maji, lakini akaondolewa baada ya wiki tatu na kupelekwa kusimamia barabara ambako ameonyesha uwezo mkubwa, iweje kwa wabunge?” alihoji Ngeleja.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema mabadiliko yanayofanywa hayawezi kuleta tija katika bunge hilo, kwani watu wanashindwa kujipanga vyema kwa kuwa hawajui kesho itakuwaje.
Lugola alihoji juu ya mafunzo waliyopata kila kamati, lakini wanabadilishwa bila utaratibu huku akisema hata kamati ya uongozi inaathirika zaidi, kwani wanapobadilishwa na kuondolewa wenyeviti lazima kamati ya uongozi ibadilike.

Mtazamo wa wadau
Damian Shumbusho, Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema Spika Ndugai anapaswa kufahamu mabadiliko ya haraka hayana tija, ikizingatiwa wabunge wanatakiwa kupata uzoefu siku hadi siku kuongeza ufanisi.
Alisema kinachoonekana kwa sasa ni Bunge kutaka kwenda na kasi ya Serikali, jambo linaloifanya waishie kufanya mabadiliko ya mara kwa mara yasiyo na tija.
Spika Ndugai hakupatikana jana kueleza kwa kina mabadiliko hayo. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema siyo msemaji na Ndugai na ndiye angepaswa kuulizwa jambo hilo.
Katika taarifa hiyo ya Bunge, Spika Ndugai aliwataka wajumbe wa kamati sita ambazo hazina viongozi kuwachagua mapema iwezekanavyo kama kanuni za Bunge zinavyohitaji.
Kamati hizo ni Hesabu za Serikali (PAC) Mwenyekiti; Kamati ya Nishati na Madini, (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (Mwenyekiti) na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Makamu Mwenyekiti.
Share:

MAAJABU, NYUMBA INAUZWA PAMOJA NA MKE WA BURE


Sleman (Indonesia) (AFP) – Tangazo la kuuza nyumba huko Indonesia liko kwenye mtandao baada ya mwanamke mwenye kuiuza nyumba hiyo kutoa maelezo ya ziada ya kukubali kuolewa na mnunuzi atakayejitokeza bila malipo ya zaidi. 
Tangazo hilo kama lilivyo katika mtandao linatoa sifa ya nyumba hiyo, ni ya ghorofa moja ikiwa na vyumba viwili vya kulala, bafu mbili, sehemu ya kuegesha magari na bwawa la samaki.
Pia tangazo hilo linatoa ‘ofa isiyokuwa ya kawaida’ kwa mnunuzi – “Ukinunua nyumba hii, unaweza kumuomba kumuoa mwenye nyumba”, pembezoni mwa nyumba hiyo kuna picha ya Wina Lia mjane wa miaka 40 ambaye pia ni mmilki wa saloni akiwa ameegemea kwenye gari mbele ya nyumba hiyo.
Tangazo hilo limesema kwamba vigezo na masharti vinapaswa kuzingatiwa, na kutilia makazo kwamba ofa hiyo ni “Kwa ajili ya wanunuzi wa kweli na haijadiliwi”. Nyumba hiyo iliyopo Sleman katika kisiwa cha Java, inauzwa kwa rupia milioni 999 (sawa na dola 75,000).
Taarifa ya ofa hiyo ilienea haraka sana miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ya Indonesia.
Mtumiaji anayejulikana kwa Bodies99 katika jukwaa la Kaskus, amesema kwamba Lia “amekuwa mjanja – licha ya kwamba nyumba hiyo itauzwa lakini bado atabaki kuwa mmiliki.”
Lia ameimbia AFP kwamba “ameshtushwa na yaliyojitokeza”, kwani ameshangazwa na idadi kubwa ya waandishi wa wanakwenda kumohji, na polisi, Waislamu walio wengi katika nchi hiyo pia wanaumuuliza maswali.
Polisi walikuja “kuthibitisha habari hiyo kwani tangazo si la kawaida. Lakini niliwafamaisha kwamba hilo halikuwa wazo langu.” Alisema.
Mama huyo mwenye watoto wawili alieleza kwamba alimuomba rafiki yake ambaye ni wakala wa uuzaji majumba amsaidia kupata mnunuzi na wakati huo huo kumtafutia mchumba, na alitegemea kwamba angewasilana na baadhi ya watu kuhusiana na kadhia hiyo na hakutegemea kama ingewekwa kwenye mtandao.
“Nilimwambia rafiki yangu ambaye anafanya kazi kama wakala wa uuzaji wa nyumba kwamba kama kuna mnunuzi ambaye ni hajaoa au amefiwa na mkea anayetaka kununua nyumba ambaye kwa wakati huo huo anatafuta mchumba anaweza kunifahamisha kwani name ni mjane,” alisema.
Amesema kwamba kuna mnunuzi mmoja ambaye wa kweli aliyejitokeza siku ya Jumatano lakini akakataa kutoa maelezo zaidi.
Share:

KUFUATIA TANGAZO LA KUZIMA SIMU FEKI TZ, ZAZIDI KUPUNGUA NCHINI


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zimeendelea kupungua kutoka asilimia 30 mwezi Desemba hadi kufikia asilimia 13, Machi mwaka huu.
Kutokana na kupungua huko, inamaanisha kwamba simu feki nchini zinazidi kupungua.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA James Kiraba amesema katika uchambuzi na matokeo ya awali ambacho pia kilishirikisha kampuni za mawasiliano kimeonyesha kuwa mwezi Februari ilishuka mpaka asilimia 18.
Amesema uchambuzi wa Februari ulionyesha idadi ya namba tambulishi ambazo hazikuwa na viwango zilikuwa asilimia tatu, vilevile idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa na asilimia 18, huku simu halisi zikiwa asilimia 79.
"Uchambuzi wa Machi unaonyesha idadi ya namba tambulishi ambazo hazina viwango zilikuwa sawa na asilimia mme, huku idadi ya namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa asilimia 13. Uchambuzi huu unahusisha kampuni zote za simu nchini," amesema Kiraba.
Share:

MAPATO YA MADINI YAONGEZEKA TZ, BIL 6 HUPOTEA KILA MWAKA


Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji wa Uwazi Katika Mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (Teiti), Jaji Mark Bomani amesema bado Serikali inapoteza Sh6 bilioni kila mwaka katika mapato ya madini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa ripoti ya tano na sita za Teiti, Jaji Bomani alisema kiasi hicho kimepungua kutoka Sh66 bilioni zilizokuwa zikipotea hadi kufikia mwaka 2009, ilipotolewa ripoti ya kwanza ya kamati hiyo.
“Kwanza nakshi kati ya malipo yaliyosemekana yamefanywa na kampuni na fedha zilizokuwa zimepokelewa na Serikali, imezidi kupungua. Ripoti ya kwanza ya mwaka 2009 ilionyesha nakshi ya Dola za Marekani 30 milioni (Sh66 bilioni). Hii ilitushtua sana,” alisema Jaji Bomani na kuongeza:
“Angalau ripoti ya mwaka 2014 nakshi imeshuka hadi kufikia Sh6 bilioni. Jumla ya mapato ya Serikali yamepanda kutoka Sh28 bilioni hadi Sh1.2 trilioni, yaani ongezeko la takribani mara 10.”
Hata hivyo alisema licha ya ongezeko hilo bado mapato yangeongezeka zaidi, kama hatua zingechukuliwa.
“Kwa mfano hadi mwaka 2012 mrabaha unaotolewa na kampuni za madini ya dhahabu ulikuwa asilimia tatu. Kamati yangu ilipendekeza…kwanza asilimia ya mrahaba iongezwe kutoka asilimia tatu hadi angalau asilimia tano. Pili, mrabaha usiwe faida zilizopata hizo kampuni, bali jumla ya mauzo. Tofauti yake ni kubwa mno,” alisema Jaji Bomani.
Aliongeza kuwa Serikali ilitekeleza ushauri huo na kupandisha mrabaha huo, kutoka asilimia tatu hadi nne.
Hata hivyo alisema pendekezo lao la kutaka asilimia 60 ya mauzo ya kampuni za madini yarejeshwe nchini, halikukubaliwa.
“Kampuni za madini ya dhahabu kwenye mikataba maalumu ziliruhusiwa kuwekeza nje mauzo yake yao yote, kinyume na utaratibu wa kampuni nyingine ambazo hutakiwa kurejesha nchini mauzo yao,” alisema.
Alisema kwa bahati mbaya zaidi ruhusa hiyo imerasimishwa katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.
“Utaratibu huu umeinyima Tanzania fursa ya kuongeza fedha za kigeni (foreign reserves) jambo linalochangia kuimarisha thamani ya shilingi. Naishauri Serikali kulitafakari suala hili hasa kwa kujua kwamba ni asilimia 20 tu ya madini yaliyogunduliwa ndiyo inachimbwa hadi leo. Bado asilimia 80 hayajachimbwa.”
Jaji Bomani ambaye alitumia fursa hiyo kustaafu nafasi yake ya uenyekiti wa kamati hiyo, aliishauri pia Serikali kupanua wigo wa wachimba madini kama vile wachimbaji wa kati ambao pato lao linazidi Sh200 milioni.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu, Ludovick Utouh aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ripoti hizo, alisema Serikali ilifanya makosa kuzimilikisha kampuni za madini migodi moja kwa moja.
‘Tunaweza kupata mapato zaidi ya madini kama tutaangalia umiliki. Mimi kama Utouh nasema utaratibu tulioutumia haukuwa sahihi. Botswana kwa mfano, ile dhana ya kusema Serikali haifanyi biashara haipo. Inatakiwa ifanye biashara kwa niaba ya wananchi wake. Tunatakiwa kuwa na wawakilishi wetu kwenye kampuni hizo, hata kwenye bodi zao,” alisema Utouh.
Alisema kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda rasilimali za nchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano kifungu cha 27 kinasema, kila mtu ana wajibu wa kutunza rasilimali za nchi… haya yanayozungumzwa hapa ni ya kisheria,” alisema Utouh.

Share:

ESCROW, HATIFUNGANI YA STANBIC VYAIBUKA TENA BUNGENI




Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe jana aliibua mambo mazito bungeni wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Rais –Tamisemi na Utawala Bora, likiwamo la ukiukwaji wa Sheria ya Bajeti kutokana Bunge kupitisha bajeti Sh23.7 trilioni huku Serikali ikija na bajeti ya Sh29 trilioni.
Mambo mengine yaliyobainishwa na mbunge huyo ni sakata la ufisadi wa hati fungani ya Sh1.2 trilioni katika Benki ya Standard ya Uingereza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kushindwa kutoa majibu ya uchunguzi wa miamala kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow kwenda Benki ya Stanbic.
Kuhusu bajeti, Zitto alisema kuna ukiukwaji wa Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 katika mchakato wa bajeti ya mwaka 2016/17 kwamba kifungu cha 8 cha sheria hiyo kinaeleza namna ambavyo mfumo wa bajeti ya Serikali unapaswa kuwa.
“Vifungu cha 8(1)(b) na 9(1)(a) na 19(1) vinataka ‘mpango na miongozo ya bajeti’ ipitishwe na Bunge katika mkutano wake wa Februari kila mwaka. Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango na kupitisha Mpango wa Bajeti uliokuwa na Bajeti ya Sh23.7 trilioni,” alisema.
Alisema kiasi hicho ni tofauti na bajeti inayojadiliwa sasa ya Sh29.5 trilioni na kubainisha kuwa jambo hilo si utawala bora kwa maelezo kuwa utungaji wa bajeti umeainishwa kisheria na kama sheria hazifuatwi, ni vigumu hata Bajeti yenyewe kutekelezwa.
“Ili kurekebisha hali hii ni lazima Bunge likae tena kama kamati ya mipango na kupitisha upya viwango vya juu vya bajeti kabla ya mjadala wa bajeti kuendelea au angalau kabla ya kupitisha bajeti kuu, Juni 2016,” alisema na kwamba bajeti za taasisi hazimo kwenye vitabu vya bajeti ya Serikali kinyume na sheria ya bajeti.
Kuhusu ufisadi wa Sh1.2 trilioni, mbunge huyo alisema mwaka 2013, Serikali ilikopa fedha hizo kutoka nje kwa msaada wa Benki ya Standard ya Uingereza ambayo sasa inaitwa Standard Bank, kwamba mkopo huo wenye riba inayoweza kupanda umeanza kulipwa Machi mwaka huu.
Alisema mkopo huo utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa inayolingana na kuongeza kuwa mkopo huo umegubikwa na ufisadi huku baadhi ya Watanzania wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani wakihusishwa na sehemu ya mkopo huo.
“Jambo la kushangaza ni kwamba wanaosemekana kula rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Vilevile, waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Waliopo mahakamani ni wanaosemekana kutumika kupeleka rushwa. “Mjumbe kashtakiwa, lakini aliyemtuma hajashtakiwa na aliyepelekewa kilichotumwa hajashtakiwa. Hapa kuna tatizo la msingi ambalo tukilitatua Serikali yetu itaepuka masuala kama haya siku za usoni.”
Alisema ana barua ya kundi la Watanzania zaidi ya 2,000 wakitaka benki hiyo ya Uingereza ichunguzwe katika suala hilo la hati fungani huku Takukuru ikitumia taarifa ya Taasisi ya Uingereza ya (SFO) katika kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hilo.
Alisema SFO haikufanya uchunguzi dhidi ya benki hiyo ya Uingereza na kushangazwa na Tanzania kusaidiwa kesi hiyo na wataalamu kutoka nchi hiyo.
“Iwapo tutafanikiwa kuonyesha kuwa Benki ya Standard ilihonga kupata biashara nchini kwetu, Tanzania itakuwa fundisho kwa kampuni ya kimataifa kwamba Afrika siyo mahala pa kuhonga na Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake na tutaokoa zaidi ya Sh2 trilioni katika deni la Taifa,” alisema.
Share:

ZITTO: WAHUSIKA 'ESCROW' WABURUZWE KORTINI


MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo) ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwafikisha mahakamani wahusika wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow ili sheria ichukue mkondo wake.
Zitto aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana wakati akichangia kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, iliyowasilishwa na Waziri Angela Kairuki pamoja na ile ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyowasilishwa na Waziri wake, George Simbachawene.
Alisema mwaka 2014, Takukuru waliijulisha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwamba ilikuwa inachunguza na kumaliza uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenda Benki ya Stanbic Tanzania.
Alisema katika taarifa zote ambazo Takukuru inatoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna mahali inapozungumzia maendeleo ya suala hilo. “Hata siku moja hakuna mahala Takukuru wanasema kuhusu uchunguzi huu na lini wahusika waliochota fedha za umma watafikishwa mahakamani.
Naomba tupate kauli ya serikali kuhusu jambo hili kwani ni moja ya jipu,” alisema Zitto ambaye aligusia suala la ukiukwaji wa Sheria ya Bajeti. Alisema kuna ukiukwaji kadhaa wa sheria ya bajeti kama vile sheria namba 11 ya mwaka 2015, ambapo kifungu cha 8 cha sheria hiyo kinaeleza namna ambavyo mfumo wa Bajeti ya Serikali unapaswa kuwa.
“Vifungu vya 8(1)(b) na 9(1)(a) na 19(1) vinaeleza namna mchakato wa bajeti unavyopaswa kuwa. Vifungu hivi vinataka mpango na miongozo ya bajeti ipitishwe na Bunge katika mkutano wake wa Mwezi Februari kila mwaka.
Share:

SERIKALI KUPELEKA 'BAADHI' YA MIKATABA BUNGENI


SERIKALI imesema ipo tayari kuwasilisha bungeni baadhi ya mikataba ambayo itaonekana ina ulazima wa kufika bungeni ili kujadiliwa na wabunge kwa niaba ya wananchi kabla ya kupitishwa.
Hayo yalisemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Kunti Majala (Chadema) aliyetaka kufahamu ni kwa nini serikali inapitisha mikataba bila kuiwasilisha bungeni.
Katika swali lake, Majala alisema kinyume cha matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoagiza mikataba kufikishwa bungeni ili kujadiliwa, serikali imekuwa ikipitisha mikataba hiyo bila kufanya hivyo.
Alisema pamoja na madhara mbalimbali, yanayosababishwa na hatua hiyo, pia nchi imekuwa inapata hasara kubwa kutokana na baadhi ya watendaji kupitisha mikataba hiyo kwa kushawishika na rushwa, hatua aliyosema imechangia kushamiri kwa vitendo vya ufisadi nchini.
Waziri Mkuu akijibu swali hilo, alikiri kuwa ni kweli Bunge lina wajibu wa kuisimamia serikali lakini yapo maeneo ambayo limetoa mamlaka ya kisheria kwa serikali kutekeleza majukumu mbalimbali ili kuharakisha maendeleo.
Alisema moja ya eneo ambalo wabunge kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametoa mamlaka kwa serikali kutekeleza majukumu yake ni katika eneo la mikataba, kwa Katiba kutoa nguvu ya kisheria kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia na kupitisha mikataba hiyo.
“Mwanasheria Mkuu anafanya kazi hii ya kupitia mikataba kwa niaba ya serikali na Bunge, kama mikataba yote ingekuwa inakuja hapa bungeni ili kujadiliwa na wabunge basi Bunge lisingekuwa na kazi nyingine zaidi ya kupitia mikataba,” alisema Waziri Mkuu, Majaliwa.
Alisema hata hivyo hakuna ubaya, endapo wabunge watapendekeza kuwasilisha bungeni mikataba ya kiwango au aina fulani ili ijadiliwe na wabunge kwa niaba ya wananchi ili kulinda maslahi mapana ya taifa.
Kuhusu ufisadi katika mikataba, Waziri Mkuu alisema pamoja na mikataba kupitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pale inapobainika kuwepo kwa ukiukaji wa maadili na sheria za nchi, hatua mbalimbali zimekuwa zinachukuliwa kwa wahusika wa suala hilo
Share:

UTENGUZI WA BOSI TIC WAZUA MIJADALA


Baada ya Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Juliet Kairuki, mjadala umeibuka kuhusu kitendo cha mkurugenzi huyo mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kutochukua mshahara tangu mwaka 2013 alipoteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Kitendo hicho kimetajwa kuwa moja ya sababu za kutimuliwa kwake.
Swali hilo na sababu tofauti za uamuzi huo ndizo zilizotawala mijadala mbalimbali kwa siku nzima ya jana, ikiongozwa na mitandao ya kijamii.
Rais Magufuli alitangaza uamuzi wa kutengua uteuzi wa Kairuki Alhamisi ya jana akisema uamuzi huo ulifanywa tangu Aprili 24 na kwamba moja ya sababu za kuondolewa kwake ni kutochukua mshahara tangu Aprili, 2013.
“Pamoja na mambo mengine, hatua hii imechukuliwa baada ya Mheshimiwa Rais kupata taarifa kuwa Bibi Kairuki amekuwa hachukui mshahara wa Serikali tangu alipoajiriwa Aprili 2013 mpaka sasa, jambo linalozua maswali mengi,” inasema taarifa ya Profesa Adolf Mkenda, katibu mkuu wa Biashara na Uwekezaji wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Tofauti na watumishi wengine waandamizi ambao baada ya uteuzi wao kutenguliwa Ikulu ilisema watapangiwa kazi nyingine, kwa Kairuki atapangiwa kazi nyingine iwapo atataka kuendelea kufanya kazi serikalini.Awali ilishawahi kuripotiwa katika vyombo vya habari kuwa Kairuki alikuwa hachukui mshahara uliotajwa kuwa Sh5 milioni (ambao Mwananchi haijaweza kuthibitisha) unaotolewa na TIC kwa kuwa ni mdogo kulinganisha na aliokuwa akipata nchini Afrika Kusini kabla ya kuombwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuja nchini kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.
Kabla ya kuteuliwa na Kikwete kushika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Emmanuel Ole Naiko kustaafu, Kairuki alikuwa akifanya kazi Afrika Kusini katika chama cha benki cha Afrika Kusini, akiwa meneja mkuu wa Idara ya Benki na Huduma za Fedha.
Inadaiwa kuwa akiwa TIC, Kairuki, ambaye ni mwanasheria alikuwa akipendekeza apewe mshahara wa Sh18 milioni kwa mwezi kiwango ambacho kinadaiwa kingeendana na stahiki alizokuwa akipata Afrika Kusini. Madai hayo yalipingwa na Kairuki mwaka jana.
Katika mjadala mwingine, inaelezwa kuwa pamoja na kutolipwa mishahara, Kairuki aliweza kumudu maisha kutokana na kuwa na safari nyingi zinazoendana na nafasi yake ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na hivyo kupata posho nzuri.
Kundi jingine lilieleza kwenye mijadala hiyo kuwa Kairuki alikuwa akilipwa posho zinazofikia Sh25 milioni na hivyo kuweza kumudu maisha bila ya kuchukua mshahara.
Hakuna mjadala ulioweza kuthibitisha madai hayo, lakini imeelezwa kwenye mitandao hiyo kuwa hali iligeuka baada ya Serikali kukubaliana naye mshahara na mtendaji huyo kudai malimbikizo yote ya mishahara ambayo hakulipwa.
Jitihada za kumpata Kariuki jana ziligonga mwamba.
Profesa Mkenda hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo la mshahara na mtumishi wake wa zamani.
“Mshahara wa nafasi hiyo upo na umekuwepo siku zote. Kabla yake kulikuwa na mtangulizi wake alikuwa anapokea mshahara,” alisema Profesa Mkenda kupitia ujumbe mfupi wa simu.
Alipoulizwa ni jambo gani lilitokea hadi Kairuki asichukue mshahara huo na Serikali ilichukua hatua gani za awali kumalizana naye mapema kabla ya kumalizika miaka mitatu, Profesa Mkenda hakujibu ujumbe wa swali hilo.
Lakini alisisitiza kuwa ngazi ya mshahara ya Mkurugenzi Mtendaji wa TIC ipo na haijawahi kubadilishwa tangu taasisi hiyo ianzishwe.
Hata hivyo, mwandishi wetu alipotaka ufafanuzi kutoka kwa katibu mkuu huyo iwapo mshahara ulikuwa ukiingia katika akaunti ya Kariuki halafu hautumii au haukupelekwa kabisa katika akaunti yake, hakujibu.
Katibu Mkuu Wizara ya Utumishi, Dk Laurian Ndumbaro alisema jambo hilo alikuwa amelisikia kwa mara ya kwanza mchana na kueleza kuwa Profesa Mkenda ana majibu zaidi.
Alipoombwa kuelezea iwapo kanuni au taratibu za utumishi zinambana mtu asiyechukua mshahara, aliahidi kumtafuta mwandishi kwa kuwa alikuwa bungeni lakini baadaye hakupokea tena simu.
Watu waliohojiwa na Mwananchi walikuwa na maoni tofauti.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Damian Shumbusho alisema iwapo alitenguliwa bila uchunguzi wa kina, uamuzi huo si wa busara.
Alisema kuwa iwapo kukubali kufanya kazi pasipo kuchukua mshahara ni kosa kwake na Serikali nayo inawajibika kwa kuwa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya Mwaka 2004 hairuhusu mtu kufanya kazi kabla ya makubaliano. “Hapa tatizo linaonekana lipo kwenye mkataba. Pasipo makubaliano ya mshahara mtu hawezi kufanya kazi,” alisema Shumbusho.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Nicholas Mgaya alionyesha wasiwasi wa mwajiriwa kutochukua mshahara.
“Unakula nini siku zote kama huchukui mshahara? Kwanini huchukui mshahara wako na kuutumia. Una kula rushwa au una chanzo kingine cha mapato kisichojulikana?” alihoji.
Alisema Tucta hawawezi kuzungumzia jambo lolote linalohusu wateule wa Rais kwa kuwa ana mamlaka kikatiba kutengua uteuzi wao, lakini wana uhakika Dk Magufuli alifanya uchunguzi wa kina na kushauriwa na wataalamu kabla ya hatua ya jana.
Mtaalamu wa masuala ya rasilimali watu, Elias Baraka kama wengine alihoji Kairuki alikuwa akiishi vipi bila kuchukua mshahara na kama uchunguzi umebaini hivyo ana tatizo la kukwepa uwazi.
“Kama uchunguzi umefanyika na ukabaini hivyo, ana kosa la kutokuwa mwaminifu. Hakuwa muwazi. Alikuwa anaishije bila mshahara? Hivyo adhabu hiyo itakuwa sahihi vinginevyo alitakiwa asimamishwe kwa uchunguzi zaidi,” alisema Baraka.
Wakati Profesa Mkenda akitangaza utenguzi huo, Kairuki alitakiwa kuwa mmoja wa waongozaji wa mkutano wa wawekezaji kutoka Urusi uliokuwa ukiendelea jana kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere.
Kairuki, ambaye taasisi yake ilikuwa moja ya waandaji wa mkutano huo, hakuonekana tangu asubuhi hata kabla ya tangazo la kutumbuliwa. Ratiba ya mkutano huo inaonyesha kuwa alitakiwa kuongoza mkutano huo muhimu sambamba na mwanzilishi wa kampuni ya b2b-export.com kutoka Urusi, Ekaterina Dyachenko na kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji Biashara Tanzania (Tantrade), Edwin Rutageruka.Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage aliyekuwepo katika mkutano huo, alipoulizwa kuhusu sababu ya Kairuki kutopokea mshahara na sababu za Serikali kutochukua hatua kwa miaka aliyotumikia TIC, alisema hakuwa na taarifa za kutimuliwa kwa Kairuki.

SOURCE
Share: